Health&Food

Pombe, tatizo linalosumbua jamii

on

UTUMIAJI vileo husababisha madhara na huongeza vitendo vya utumiaji mabavu, ubakaji na hata unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

Pombe ina madhara makubwa ya kimwili, kiuchumi na kijamii kuliko wengi wanavyofikiria. Moja ya madhara ya ulevi kiafya ni kushuka kwa mapigo ya moyo, jambo ambalo baadaye huweza kusababisha kifo. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 1980 asilimia 86 ya makosa ya jinai yakiwemo ya kuua na asilimia 50 ya matukio ya uporaji na kutumia nguvu yalisababishwa na ulevi. Wataalamu wa afya wanasema, pombe zenye kilevi ndani yake huwa na sifa ya kulewesha na kudhoofisha mwili.

Alkoholi katika mwili wa mwanadamu hudhoofisha sehemu za neva, yaani mshipa ya fahamu katika mwili wa mwanadamu, hali ambayo huvuruga mzunguko wa kawaida wa damu yote. Wataalamu wanasema mtu anapokunywa pombe, baada ya muda joto la mwili hupanda na kuongezeka na baadhi ya vitendo vyake huongezeka, mapigo ya moyo huenda kwa kasi. Baada ya hatua hiyo athari zake hupenya na kufikia mishipa ya ufahamu na hivyo mtumiaji kuanza kuzungumza kupita kiasi na wakati mwingine kutokuwa msikivu.

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) katika kampeni yake ya kuangalia athari za pombe katika jamii na kupunguza tatizo hilo, kilifanya mahojiano na wataalamu mbalimbali katika kuangalia ulevi na afya na kubaini kuwa uraibu (addiction habit) ni tatizo kubwa katika jamii. Mkuu wa Kitengo cha afya ya akili na dawa za kulevya katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Norman Sabuni, anasema unywaji wa pombe unaharibu sana ubongo wa mtu.

Wakati mtu anapojiona kuwa anasikia raha na kuburudika kwa pombe, huwa hana habari kuwa anaziua seli za ubongo wake. Ubongo unakosa hewa ya oksijeni na hivyo kuharibiwa, au huharibika kiasi kwamba anatumbukia katika hali ya kuchanganyikiwa akili. Dk Sabuni anasema utafiti na uzoefu wa wataalamu unaonesha kwamba, utumiaji kilevi unasababishwa na sababu mbalimbali baadhi yake ikiwa ni hali ya wasiwasi, fadhaa, msononeko na kutojiamini au jitihada za kukimbia hali ya fadhaa na kwa vijana wakati mwingi huchangiwa na mazingira au kuiga mkumbo.

“Baadhi ya watu wakati wanapokuwa na hali ya wasiwasi wakiwa na lengo la kutafuta hali ya utulivu huamua kunywa pombe au kilevi wakijidanganya kwamba, wanaweza kukwepa hali ya mawazo na hali ya msononeko wanayokabiliwa nayo. Lakini ukweli wa mambo ni kuwa, katika hatua ya awali, mlevi hupata hisia ya uongo (temporary relief), lakini baada ya muda, athari mbaya za kutumia pombe huanza kudhihirika,” anasema Dk Fredrick Mashili ambaye ni mtaalamu wa Fisiolojia ya homoni na mazoezi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Aidha, Dk Sabuni anasema utumiaji wa kilevi huleta magonjwa mabaya ya saratani ya tumbo na maini, magonjwa ya tumbo, kifua kikuu, magonjwa ya akili na tatizo kubwa sana katika jamii ni uraibu. “Shida ya uraibu linaleta ‘side effect’ kwa mtu kama hajanywa pombe haoni raha na shida kubwa ni kuwa huwezi kumuachisha mara moja mtu aliyetawaliwa na pombe kupita kiasi, kwani anaweza kupata madhara makubwa zaidi kama ataiacha ghafla kitu kama kifafa.

Akishafikia hatua hiyo ni lazima mtu huyo kwenda kituo cha afya kupatiwa tiba stahiki kwa kupewa dawa zitakazozuia madhara yatakayojitokeza,” anasema. Uraibu ndio tatizo kubwa katika jamii ambalo linachangia unyanyasaji wa kijinsia, kuparaganyika kwa ndoa na hata watoto wa mitaani. Katibu wa Mkuu wa Chama cha Madaktari wa afya ya akili, Kissah Mwambene, anasema pombe imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa unyanyasaji wa kijinsia na kubainisha kuwa takwimu za Marekani zinaonesha kuwa kati ya asilimia 55 hadi 74 ya matukio ya unyanyasaji wa kijinsia, kisababishi kikubwa ni pombe.

Mwambene anasema kwa Tanzania tafiti iliyofanywa Mkuranga Mkoa wa Pwani na Monduli, Arusha kati ya Desemba 2010 na Januari 2011, zinaonesha kuwa jumla ya watu 631 waliohojiwa Mkuranga na Monduli, walionesha kuwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ni hali ya kawaida na pombe imechangia sana vitendo hivyo. Wataalamu wa masuala ya tiba wanaamini kwamba, kuna jumla ya magonjwa 60 yanayosababishwa na unywaji wa pombe, baadhi yao yakiwa ni maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi, unene kupita kiasi, utapiamlo hasi, mimba kuharibika, kisukari, saratani, kuharibika kwa ini, figo na kadhalika.

Inasikitisha kuwa, licha ya madhara yote ya ulevi yanayoelezwa na wataalamu kwa mtu binafsi na jamii kwa ujumla, lakini kiwango cha utumiaji pombe kinazidi kuongezeka kwa kasi duniani na baadhi ya jamii hata zimefikia hatua ya kuifanya pombe kama ndio kinywaji bora cha kumkirimu mgeni. Kuhusu madhara ya kijamii, Dk Sabuni anasema pombe imechangia kusambaratisha familia, baba au mama wanaishia kutekeleza watoto na familia.

“Tunashuhudia ndoa kuvunjika, familia kusambaratika na hata watoto kutekelezwa kutokana na wazazi au baba ambaye ndiye msimamizi mkuu wa familia kuwa mraibu wa pombe na hivyo kutoitunza familia. “Utumiaji wa pombe kupita kiasi huhatarisha usalama wa uchumi wa familia na ukizingatia kuwa familia nyingi hukidhi mahitaji yake kupitia kwa baba au mama kufanya kazi au msimamizi mhusika wa familia, hivyo inapotokea wahusika hao kuwa walevi, huacha majukumu yao ya kukidhi mahitaji ya familia zao na huo huwa mwanzo wa kusambaratisha familia.

Amina Husseni anayesimamia kituo cha watoto yatima eneo la Magomeni, Dar es Salaam, anasema, katika familia mama na watoto ndio ambao huwa waathirika wakuu wa ulevi ndani ya familia. “Vitendo vibaya na utumiaji mabavu ya mume mlevi ndani ya familia humharibu kisaikolojia mke na kumfanya akate tamaa na hatimaye kutekeleza jukumu lake ndani ya familia kama mama. Katika mazingira kama hayo, mama anakuwa na mambo mawili ya kuchagua ama kurejea kwao (kuachika) au avumilie vitendo hivyo huku akiwa anaumia.

“Endapo atabaki kwa mumewe basi atachukua majukumu ya kulea familia, jambo ambalo linafanya malezi ya watoto kuwa ya upande mmoja. Pia familia ambayo ni ya walevi ni rahisi kwa watoto nao kujitumbukiza katika masuala ya ulevi au mambo mengine mabaya zaidi,” anasema.

Anapozungumzia changamoto za kudhibiti matumizi ya pombe kupita kiasi, Dk Sabuni anasema imekuwa ni shida kudhibiti unywaji huo nchini kutokana na pombe kuwa biashara kubwa yenye kipato. Anasema sheria imeelekeza muda wa kuuza pombe, nani auziwe lakini pia sheria inaipa mamlaka halmashauri kutoa leseni ambazo zimekuwa zikitoa mwanya wa uuzaji holela wa pombe.

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *