Health&Food

Chunguza dalili za kiafya

on

chunguza dalili za kiafya za mama kila anapohudhuria.

 

 • Chunguza uzito wake na shinikizo la damu.
 • Kama anajisikia kuumwa au hajisikii vizuri, pia chunguza hali
  joto yake, mpwito wa mshipa unaotoa damu moyoni, na upumuaji. Jifunze
  jinsi ya kuchunguza dalili hizi za afya kupitia Kumchunguza mgonjwa (kinaandaliwa).
 • Chunguza ukuaji wa mtoto na mkao wake tumboni na sikiliza mapigo yake ya moyo.

Uzito

Iwapo una mzani, chunguza uzito wa mama kila anapohudhuria. Anapaswa
kuongezeka uzito, kidogo kidogo kwa wakati katika kipindi chote cha
ujauzito. Kwa ujumla, mwanamke mjamzito mwenye afya nzuri huongezeka
kilogramu kati ya 12 na 16 wakati wa ujauzito. Kuanzia miezi 4, ni jambo
zuri kiafya kuongezeka chini kidogo ya nusu kilogramu kila wiki.
Kiwango cha kuongezeka kinaweza kuzidi kama ameanza ujauzito akiwa na
uzito chini ya kiwango, na kupungua kama ameanza ujauzito akiwa
amenenepa.

Kama mama haongezeki uzito, msaidie kupata chakula zaidi na kula zaidi.

Ugonjwa wa kisukari unaweza kusababisha uzito kuongezeka ghafla (angalia Magonjwa yasiyopona – kinaandaliwa).
Ongezeko ghafla la uzito katika wiki za mwisho za ujauzito nao unaweza
kusababishwa na mapacha au hali inayotangulia kifafa cha mimba.

Shinikizo la Damu

Shiniko la damu la kiwango cha 140/90 au zaidi siyo salama kiafya.
Kama kiwango cha shinikizo la damu kinazidi kupanda kila mara unapopima,
hiyo pia ni dalili ya hatari kiafya.

Shinikizo la juu la damu mwanzoni katika ujauzito huashiria
tatizo la kiafya ambalo husababishwa na ongezeko la shinikizo la damu
kwenye mishipa inayotoka kwenye moyo. Tatizo hili hujulikana kama
haipatensheni (angalia Magonjwa yasiyopona – kinaandaliwa). Ujauzito na kujifungua huwa ni hatari kwa mama mwenye tatizo la haipatensheni. Anahitaji msaada wa daktari.

Andika kiwango cha shinikizo la damu kila mara mama mjamzito anapohudhuria. Je kiwango kinapanda?

Shinikizo la juu la damu baada ya wiki 28 au miezi 6½ ya ujauzito
linaweza kuashiria hali inayotangulia kifafa cha mimba. Hili ni tatizo
la hatari ambalo linaweza kusababisha shambulio la kifafa cha mimba na
hata kupoteza maisha. Mama mjamzito atahitaji msaada wa daktari haraka.

Hali inayotangulia kifafa cha mimba

Hali inayotangulia kifafa cha mimba ni hali ya hatari ambayo
hujitokeza katika siku za mwisho wa ujauzito. Hakuna njia ya kuizuia.
Dalili zake kubwa ni shinikizo la juu la damu ambalo huzidi kuongezeka
kila wakati, na hatimaye mama kuanza kupata mashambulio-matikishiko ya
maungo ya mwili. Unaweza kuponya maisha yake kwa kuwa mwangalifu
kutambua dalili za hali hii katika kipindi kizima cha ujauzito na
kumpatia matibabu haraka anapoonesha dalili hizo.

Iwapo shinikizo lake la damu litapanda sana,au kama ataanza
kupatwa na mashambulio, dawa zinaweza kusaidia. Lakini tiba pekee ya
kuondoa tatizo hilo ni kwa mtoto kuzaliwa.

Dalili za hali inayotangulia kifafa cha mimba
 • Kiwango cha shinikizo la damu cha 140/90 au zaidi baada ya mimba kufikisha wiki 28 (takriban miezi 3 ya mwisho ya ujauzito) na
 • Protini kwenye mkojo (angalia Kumchunguza mgonjwa – kinaandaliwa).

Kama utakuta shinikizo la juu la damu katika kipindi cha mwisho cha
ujauzito, chunguza protini kwenye mkojo. Kama ana shinikizo la juu la
damu, na protini kwenye mkojo, mama atakuwa na katika hali inayotangulia
kifafa cha mimba na anahitaji msaada au hali yake inaweza kubadilika
haraka kuwa mbaya zaidi.

Kama hakuna protini kwenye mkojo, endelea kumwangalia kwa karibu
na kupima shinikizo lake la damu angalau mara moja kwa wiki. Pata msaada
wa daktari pale utakapoona dalili za hali inayotangulia kifafa cha
mimba.

Dalili kali za hali inayotangulia kifafa cha mimba au kifafa cha mimba chenyewe
 • Maumivu makali ya kichwa.
 • Kiwango cha shinikizo la damu cha 160/110 au zaidi.
 • Kuona giza-giza-mauzauza.
 • Maumivu katikati tumboni.
 • Kuvimba sana kukiwemo kuvimba usoni.
 • Kuchanganyikiwa akili.
 • Mitikishiko ya maungo.
Matibabu

Iwapo wakati wowote ule mama ataonesha dalili kali za hali
inayotangulia kifafa cha mimba, tafuta msaada wa daktari haraka. Maisha
ya mama yanakuwa katika hatari na anatakiwa kujifungua haraka
iwezekanavyo.

Choma sindano ya magneziamu salfeti gramu 5 katika kila kalio kama inavyoonyeshwa na mishale:
 • Kuwa mtulivu.
 • Kama mama anapata shambulio, mgeuze alalie upande wake mmoja.
  Hii humlinda asikose pumzi kwa kuzibwa na matapishi au mate mdomoni.
 • Kama unayo, mpatie oksijeni.
 • Kusimamisha mashambulio, mchome sindano ya magneziamu salfeti gramu 5 katika kila kalio. Rudia hii baada ya saa 4. Usimpe magneziamu salfeti kama pumzi zake ni chini ya 12 kwa dakika. (Magneziamu salfeti huja katika vipimo mbalimbali, hivyo kuwa na uhakika una kiwango sahihi.) Soma zaidi hapa.

Ukuaji wa mtoto katika tumbo la uzazi

Ujauzito unapotimiza miezi 5, tumbo la uzazi linapaswa kukaribia kwenye kitovu.

Baada ya miezi 3 ya ujauzito unapaswa kukaribia sehemu ya tumbo la
chini la mama, juu kidogo ya mfupa wa kinena. Katika hatua hii
inawezekana kuhisi mtoto aliyepo ndani ya tumbo la uzazi. Mimba
inapofikisha miezi 5 mtoto katika tumbo la uzazi atakuwa ameongezeka na
kufikia kwenye kitovu, na kundelea kukua kwa kiwango cha wastani wa
upana wa kidole kimoja kila wiki.

Kama tumbo la uzazi litakuwa kubwa zaidi au kuongezeka haraka,
mwanamke anaweza kuwa na ujauzito wa muda mrefu kuliko na matarijio
yako. Au anaweza kuwa na mapacha. Au anaweza kuwa na kisukari au tatizo
lingine la kiafya.

Kama ukubwa wa tumbo la uzazi na mtoto ndani yake vitakuwa
vikiongezeka polepole mno kuliko matarajio yako, inawezekana mama hana
ujauzito mkubwa kama unavyofikiria. Baadhi ya sababu zingine za
uongezekaji mdogo wa tumbo la uzazi na mtoto ndani yake ni kutokula
chakula cha kutosha, au mama kupatwa na madhara ya moshi au kemikali
zenye sumu.

Mkao wa mtoto tumboni

Mtoto mwanzoni wa ujauzito huhamahama ndani ya tumbo la uzazi. Mwishoni mwa ujauzito, mtoto huingia katika mkao wa kuzaliwa.

Ukipata uzoefu, unaweza kugusa na kuhisi iwapo kichwa cha mtoto
kinaangalia chini (mkao salama) au makalio ndiyo yanaangalia chini
(uzazi wa kutanguliza makalio, mkao ambao mara nyingi huwa wa matatizo).

Tumia mikono miwili na kukaza mikono kiasi. Mwambie mama apumue
nje polepole na kumaliza pumzi yake yote, wakati ukiminya vidole vyako
ndani kumhisi mtoto aliyeko ndani.

Gusa juu ya
tumbo la mama na mikono yako miwili. Je unahisi kichwa kigumu cha mtoto
chenye uwezo wa kujisogeza au kujitembeza? Au makalio laini laini?
Kamata sehemu ya mfupa wa
nyonga. Ni ngumu au laini? Unapokamata, unaweza kukitembeza kilichomo
sehemu zingine za mwili kwa uhuru?

Kama mtoto atakuwa ametanguliza makalio wakati wa muda wa kujifungua,
ni salama zaidi kujifungulia hospitali. Lakini kama unajikuta na mama
ambaye anakaribia kujifungua mtoto ambaye ametanguliza makalio, bonyeza hapa.

Mtoto aliyelala katikati ya njia ya uzazi (ambaye hajakaa
wima) hawezi kuzaliwa kupitia ukeni. Kama mtoto atakuwa amelalia upande
wakati uchungu wa uzazi unaaza, apelekwe hospitalini haraka. Huenda
operesheni ikahitajika.

Mapigo ya moyo wa mtoto

Zifikapo wiki 20 (takriban miezi 4½) ya ujauzito, unapaswa kuwa
katika hali ya kusikia mapigo ya moyo wa mtoto kwa kutumia kifaa maalum
cha kusikilizia-fetoskopu, na wiki chache baadaye kwa kutumia kifaa
kingine cha stesoskopu. Moyo wa mtoto mwenye afya huongeza na kupunguza
kasi ya mapigo lakini mapigo hubaki kati ya 120 na 160 kwa dakika. Hii
inakaribia mara 2 mapigo ya mtu mzima. Mapigo yanaweza kupungua mtoto
anapokuwa amelala. (Kama utasikia mapigo ya moyo kati ya 60 na 80,
huenda unasikiliza mapigo ya mama, na siyo ya mtoto). Tumia saa yenye
ulimi wa pili unaohesabu sekunde, au yenye uwezo wa kurekebishwa na
kuhesabu mapigo ya moyo kwa dakika moja.

Kichwa chini
Mapigo ya moyo wa mtoto husikika zaidi katika hatua hii
Kutanguliza
makalio
Mfanyakazi wa afya akimsikiliza mtoto kwa kutumia Fetoskopu kupitia tumbo la mama yake Baada ya wiki 20 za ujauzito,mapigo ya moyo wa mtoto huweza kuonesha jisi mtoto alivyokaa kwenye tumbo la mama yake.

Kama mapigo ya moyo yatabaki chini ya 120, au kwenda kasi zaidi ya
160, au wakati wote kuonekana kuwa katika kasi ile ile bila mabadiliko,
huenda mtoto ana matatizo na anahitaji msaada zaidi wa daktari.

Mwisho, kama utagundua kuwepo mapigo ya moyo mawili tofauti, huenda kuna mapacha.

Andaa mpango kwa ajili ya dharura

Kila dharura inayojitokeza wakati wa kujifungua inatibika. Kuvuja
damu, mashambulio ya kifafa, maambukizi, uchungu unaoendelea muda mrefu
bila mtoto kuzaliwa, vyote vinaweza kudhibitiwa kwa matumizi ya dawa
sahihi, au wakati mwingine kwa njia ya operesheni kwenye hospitali zenye
vifaa na watalaam wa kutosha. Tatizo hapa ni kupata huduma hii wakati
inapohitajika. Kumbuka ni nadra kupata tahadhari ya kutosha kabla jambo
baya halijatokea wakati wa uzazi. Fedha, usafiri, na ushirikiano kutoka
kwa wanafamilia na majirani vinahitaji kuandaliwa mapema hata kabla
uchungu wa uzazi haujaanza.

Wakutanishe mama mjamzito na watu wake wa karibu: mume wake, mama
mkwe, au mwingine yeyote yule, na kuamua kipi kitahitajika iwapo dharura
itatokea. Mahitaji yanaweza kujumuisha:

 • Kutumia gari la mtu Fulani au gari lingine.
 • Fedha za kulipia huduma za hospitali.
 • Kupata ruhusa mapema kutoka kwa wanaofanya maamuzi katika familia.

Kama upo mbali na kituo cha afya au hospitali, kwa wiki chache
zitakazokuwa zimebaki kujifungua, fikiria kuhamia kwa ndugu au jamaa
anayeishi karibu na hospitali.

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *